Kikwete anahukumiwa bure nyumba za tope Tanzania

MOJA kati ya mambo yanayosemekana ni kipimo kizuri kwa mtu kuondokana kwenye umasikini ni pamoja na kuwa na makazi bora. Nyumba bora zinatusaidia kutufanya tuonekane kwamba tumeondoka kwenye umasikini. 

Watu wengi wanaamini hivyo kwamba mtu ukijenga nyumba bora kabisa, nyumba ya matofali na ambayo imefunikwa kwa mabati ya kisasa, basi wewe utakuwa umendoka kwenye orodha ya watu ambao ni masikini. Lakini umasikini una njia nyingi za kuzungumzia. 

Kama tukiamua kuacha uvivu na kuzungumzia umasikini, tunaweza kumaliza hata kurasa za gazeti hili kutaja vyanzo na viashiria vya umasikini. Katika maisha ya kawaida kabisa ya binadamu, hakuna umasikini mbaya kama umasikini wa mawazo. 

Rais wa kwanza na baba wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amewahi kusema kwamba umasikini wa mawazo ndio umasikini mbaya zaidi. kuliko kukosa chakula, kukosa nguo, kukosa nyumba bora ya kuishi, na mahitaji mengine muhimu ni, lakini umasikini wa kushindwa kujua baya na zuri unaweza kuwa umasikini mkubwa zaidi na wa hatari katika siku zetu za kuishi hapa duniani.

Dunia hii imebadilika sana na utandawazi umetufanya kila mmoja kuwa na uhuru wa kutoa mawazo yake hata kama si kwa njia sahihi. Mitandao ya kijamii imekuwa eneo ambalo watu wanatoa maoni yao, wanaisema serikali, wanaisifia, wanatukana na wengine wanashangilia hata mambo ambayo yanayoumiza, ama kinyume chake.

 Moja ya taarifa ambayo inasambaa sana kwenye mitandao hiyo hasa twitter ni picha ambayo inaonekana kwenye ukurasa wa twitter wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Adv. Ridhiwani Kikwete akiwa katika kata ya Kimange wilaya ya Chalinze mkoani Pwani akiwa anazungumza na wananchi wake. 

Ridhiwani, ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze. "Tumefanya ziara Kata ya Kimange. Tumezungumza na wananchi na kukagua shughuli za maendeleo. Tumetumia nafasi hii kueleza shughuli zinazofanywa na serikali, mipango ya maendeleo na hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kutatua kero za wananchi wetu", ameandika Mbunge huyo katika ukurasa wake.

Ridhiwani ambaye sasa amehamishiwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama Naibu Waziri wa wizara hiypo, amekuwa na utamaduni huo, kila akipita kwenye maeneo ya jimbo lake anatumia mitandao ya kijamii kuwaonesha watu kazi anayoifanya. Na kusema ukweli pamoja na nongwa zetu za kila siku, Mbunge huyu ni mmoja wa Wabunge wanaotembelea sana wananchi wao. Chanda chema huvikwa pete.

 Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wamekosoa picha hizo, na wengine kufika mbali kwamba kwanini Mbunge huyo ambaye ni Naibu Waziri mwenye dhamana ya nyumba kuposti picha ambayo amekaa nje ya nyumba ya tope. Wanasema kwamba siyo fahari kupiga picha kwa Naibu Waziri huyo akiwa amekaa nje ya nyumba ya tope na kuiweka kwenye ukurasa wake, kwamba eti kuwa na nyumba za tope hapa nchini ni umasikini ambao umeshindwa kuondolewa hata katika kipindi ambacho Baba yake mbunge huyo, Dkt Jakaya Kikwete akiwa Rais wa nchi hii.

 Ni kweli tunaweza kusema kwamba kama nchi hatujafanya kampeni ya kutosha ya kutuondoa kwenye nyumba za tope na zile za nyasi. Lakini sio kweli kwamba Dkt Jakaya Kikwete akiwa Rais hajafanya lolote kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na makazi bora. Sio sahihi pia kumlaumu Ridhiwani kwamba katika kipindi hiki kidogo akiwa Naibu Waziri anaweza kuiondoa Tanzania kwenye kero ya nyumba za tope siyo tu kwenye Jimbo lake bali pia nchi nzima.

 Pengine tunafikiri tofauti sana. Kwa wanaofuatilia mambo ya nchi hii, ni katika uongozi wake Rais Kikwete alijitajidi sana kuhimiza kwanza matumizi bora ya ardhi, lakini pia kuhakikisha kwamba kila mtanzania anafaidika na ardhi iliyopo hapa nchini. Ni wakati wake alipambana na migogoro ya wakulima na wafugaji, akitaka kila mmoja anufaike na kuitumia ardhi yetu kwa manufaa sahihi. Lakini Dkt Kikwete tunayemlaumu leo alihimiza sana watanzania kuwa na makazi bora, na kusema ukweli nchi hii imebadilika sana. 

Tanzania ya miaka ya sitini na sabini siyo Tanzania ya sasa. Ni makosa makubwa kusema kwamba nchi hii haijaendelea. Mbunge huyo wa Chalinze anayeshutumiwa leo amezaliwa mwaka 1979, wakati nchi hii ikiwa na mambo mengi na ikiwa imepita kwenye vipindi vigumu. Nchi hii ilikuwa na mikakati mikubwa ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na maisha bora, bahati mbaya pia nchi hii imepita kwenye vipindi vigumu ambavyo kwa namna moja ama nyingine vimeyumbisha uchumi wetu.

 Lazima tukubali pia kwamba kuna maamuzi ambayo tumefanya huko nyuma yalisaidia sana kuhakikisha Watanzania wanakuwa na makazi bora. Kwa mfano, tulipokuwa na Benki ya Nyumba (THB), Watanzania wengi wanaoishi mijini waliweza kumiliki nyumba bora kutokana na mikopo ya benki hiyo. Lakini waiofaidika zaidi ni wale waliokuwa wanaishi mijini, siyo wakulima wa Vijijini.

 Leo hii hata ukiirejesha Benki ya Nyumba haiwezi kufanya kazi yake vizuri, kwani mifumo ya nchi imebadilika sana, kama ambavyo Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB) ililazimika kubadilishwa mifumo yake ili kwenda na wakati, vinginevyo nayo ingekufa.

 Kwahiyo, wale wanaosema ni aibu kwa Mbunge huyo kupiga picha akiwa na wanachi wake wanaoishi kwenye nyumba za tope wanatakiwa kufahamu kwamba kuondoa nyumba za tope si kazi rahisi ambayo inaweza kufanywa na mtu mmoja, ana awamu moja ya uongozi. Mwalimu Nyerere ameongoza nchi hii kwa miaka 24 hakuweza kuiondoa nchi yetu katika umasikini wa makazi. Ingawaje ni yeye aliyefanya kazi kubwa zaidi ikiwa ni pamoja na mawazo yake hayo ya kuanzisha benki ya nyumba. Alhaji Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa, Dkt Jakaya Kikwete, Hayati Dkt John Magufuli kila mmoja kwa wakati wake alipambana vile alivyoweza lakini si rahisi kumaliza umasikini katika nchi hii. Hata leo Dkt Samia Suluhu Hassan atamaliza muda wake wa Urais yeye na mawaziri wake hawa akina Ridhiwani, bado Tanzania itakuwa masikini katika maeneo mengi. Ni mawazo mgando pia kumlaumu Ridhiwani kwamba kwanini anatuma picha akiwa kwenye nyumba za tope. Hivi tunataka kusema kwamba nyumba za tope Tanzania zipo kwenye Jimbo la Chalinze tu? 

Ama tunataka kuaminisha watanzania kwamba sisi ndiyo masikini zaidi duniani kwamba nyumba za tope hazipo katika nchi nyingine iwe barani Afrika na kwingineko duniani? India ambako wafanyabiashara wengi hapa Tanzania wanatoka ama asili yao ni huko, ni moja ya nchi ambayo wananchi wanaishi kwenye makazi duni kabisa. Nchi nyingine kwa mujibu wa Benki ya Dunia, wananchi wake wanaishi kwenye nyumba duni zaidi ni Bangladesh, Nigeria, 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ethiopia. Hizi ndizo nchi tano ambazo zinaongoza duniani kwa kuwa na nyumba duni zaidi. Sasa unawezaje hata kuifananisha Tanzania na India, moja ya nchi kubwa kabisa duniani? Nigeria pamoja na utajiri wake wa mafuta katika Afrika lakini kuna nyumba nyingi duni. DRC pamoja na utajiri wake madini mengi, bado wananchi wake wengi wanaishi kwenye nyumba za tope. Sisi tumeoiga hatua sana, tunastahili kujipongeza badala ya kujilaani. 

Kwangu mimi nampongeza sana Mhe. Ridhiwani kwa kuonesha uhalisia wa maisha ya Jimbo lake. Na utakuwa ni uongo mkubwa tukisema kwamba hakuna Jimbo lolote hapa nchini ambako hakuna makazi duni. Tuliozaliwa vijijini tunajua hivyo, na nchi yetu iko hivyo, japokuwa mabadiliko ya makazi yamekuwa yakienda kwa kasi sana. Chalinze ni Jimbo ambalo lilikuwa sehemu ya wilaya ya Bagamoyo kwa miaka mingi. 

Wanaoifahamu wilaya hii mpya wanajua kwamba imepiga hatua kubwa kiasi kwamba kuna watu kutoka wilaya nyingine wanakwenda Chalinze na kununua Viwanja na kujenga nyumba za kuishi huko. Huu unatosha kuwa ushahidi kwamba kwenye Jimbo hilo kuna mambo mengi yamebadilika na hizi nyumba za tope zilizopo katika baadhi ya vijiji haziwezi kuondoka haraka kama ambavyo baadhi ya watu tunaaminishwa. 

Nyumba hizi zilikuwepo, zipo na zitakuwepo tu. Kwa nafasi yangu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini, nimeweza kutembea maeneo mengi hapa nchini. Nimeona jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa kuhakikisha kwamba Watanzania wanaondokana na umasikini, japokuwa kuna ukweli kwamba katika baadhi ya maeneo tuna umasikini ambao ni wa kujitakia tu. 

Hata hilo suala la kuwa na makazi bora ni jambo ambalo linamhusu mtu mmoja mmoja. Jukumu la serikali si kuwajengea nyumba wananchi wake, bali kuwapa huduma bora ambazo zitasaidia kuwa na mwamko wa kujenga nyumba bora. Kama eneo lina mazao ya kibiashara kwa mfano, na serikali imepeleka huduma muhimu huko kama masoko na barabara nzuri, wakazi wa eneo hilo wataendelea tu.