MWANGA, Kilimanjaro
Hali ya sitofahamu imeikumba shule ya msingi Jipe iliyoko wiliya ya Mwanga mkoani kilimanjaro baada ya kutokea kile kinachosemekana ni mauza uza kwa walimu.
Mauza uza yasiyofahamika yanadaiwa kuwakumba baadhi ya walimu wa Shule hiyo.
Habari zinadai kwamba baadhi ya walimu wameomba kuhamishiwa shule kutokana na mauzauza hayo ambayo yanahusishwa na imani za kishirikina.
Mtoa habari wetu anasema kwamba walimu kadhaa wameomba kuondoka shuleni hapo baada ya kukutana na mikasa ambayo haivumiliki.
“Mwalimu mmoja alijikuta amelala juu ya mgongo wa kiboko katikati ya Ziwa Jipe. Ilibidi watu watumie mtumbwi kwenda kumuokoa. Sasa fikiria, mtu amelala nyumbani kwake anajikuta ameamkia ziwani” alisikika mkazi mmoja wa maeneo hayo ambaye hakutaka kujitambulisha.
Amesema walimu wengine wamejikuta wakiamka asubuhi wanaumwa baada ya kupigwa fimbo na watu wasiojulikana usiku kucha.
“Kuna mambo mengine ambayo walimu wanafanyiwa hatuwezi kuyasema hapa, lakini ni shule ambayo imejaa mauzauza na viongozi wa Halmshauri wanajua kinachoendelea ndiyo maana wale wanaoomba kuhamishwa wanawapa kibali cha kuhama” amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Mwajuma Nasombe hakuweza kupatikana kwa njia ya simu mara kadhaa, kuzungumzia kadhia hiyo.
Hata hivyo, Ofisa Mmoja wa Halmashauri hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi amekiri kwamba kumekuwa na mauzauza makubwa katika shule hiyo.
“Hali ni mbaya, ndiyo maana unasikia kwamba walimu wanaondoka. Sisi kama Halmshauri tunajua yanayofanyika lakini kwavile ni mambo ambayo hayaonekani kwa macho tunakuwa hatuna njia ya kufanya.
Hata hivyo tunatafuta namna ya kuwashirikisha wakazi wa eneo husika kujua nini kifanyike ili amani iweze kurejea” amesema Ofisa huyo.
0 Comments