Walinzi wa kampuni ya ulinzi ya GardaWorld, wamekamatwa wakiwa katika ofisi za kampuni hiyo mkoa Mbeya, wakiwa na madawa ya kulevya aina ya bangi yenye ujazo wa nusu gunia.
Tukio hilo lilitokea Februari 23, mwaka huu majira ya saa 11 jioni walinzi wa kampuni hiyo waliofahamika kwa majina ya Brown Jerry na Issaya Mwakalinga walikamatwa na polisi na kufikishwa katika kituo cha kati mkoa wa Mbeya.
Kwa mujibu wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambao hawakupenda kutajwa majina yao walisema walinzi hao walikutwa na bangi nusu gunia ikiwa kavu na nyingine ilikuwa mbichi.
Afisa Rasilimali Watu (HR) wa kampuni hiyo, aliyefahamika kwa jina moja la Pamela, alipoulizwa kuthibitisha tukio hilo, alisema yeye sio msemaji wa kampuni na kuelekeza kwa mtu mwingine ambaye hata yeye alipopigiwa simu alishindwa kuthibitisha habari hizi.
Alisema, "mimi siwezi kuzungumza lolote kuhusu suala hilo kama unataka ufafanuzi mzuri fika makao makuu yalioko maeneo ya kwa Rais Mwinyi Msasani" alikata simu na alipopigiwa tena hakupokea simu.
Kamanda wa Polisi mkoa Mbeya, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ACP Benjamin Kuzaga, alipoulizwa kuhusu tukio hilo hakuweza kuzungumza kwa kuwa hakuwa na taarifa na tukio hilo.
"Sina taarifa ya tukio hilo.....nipe dakika moja ntakurudia, "alisema ACP Kazaga na kumuunganisha mwandishi wa habari hizi na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mbeya ambaye nae hakuweza kutoa taarifa zaidi na kuahidi kufuatilia na kutoa ufafanuzi badae.
Hata hivyo, meneja wa kampuni ya GardaWorld Mbeya hakuweza kupatikana kuthibitisha taarifa hizi, licha ya kupigiwa simu mara kadhaa simu yake inaita muda mrefu bila kupokelewa.
0 Comments