Mtu mmoja asiyejulikana ametelekeza madawa aina ya bangi, kwenye ofisi za kampuni ya ulinzi ya GardaWorld mkoa wa Mbeya.
Hayo yamesemwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, walipokuwa wanatoa ufafanuzi kufuatia tukio la walinzi wawili wa kampuni hiyo kukamatwa kwa madai ya kukutwa na bangi nusu gunia.
"Sio kiasi hicho kinachotajwa namna ilivyokuwa kunasemekana kuna mtu alitumwa kwenda kwenye zile ofisi za kampuni ya ulinzi alikuwa na bahasha", alisema
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa Mbeya, (RCO), kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa Mbeya, Kamishina Msaidizi wa Polisi, (ACP), Benjamin Kusaga.
Alisema wasaidizi wahudumu wa ofisi hiyo walipokea bahasha hiyo kwa mtu wasiomjua wakiwa hawajui kilichopo ndani, lakini baadae walipokuja viongozi wao waliifungua na kubaini kuwa kulikuwa na kete za bangi.
Alisema ",wao wenyewe ndio walikwenda polisi wakasema kuna mtu kawaletea bahasha baada ya kufungua wakakuta baadhi ya kete za bangi."
Kamanda Kusaga anasema wanaendelea kupeleleza tukio hilo kujua nani aliyeleta hiyo bahasha na alikuwa na malengo gani kupeleka bangi kwenye ofisi za kampuni hiyo.
"Tunaendelea kuchunguza bangi iliyokamatwa inabidi tuipeleke kwa Mkemia tujilidhishe kweli ni bangi au ni kitu gani....kiukweli hata wale walioleta hiyo bangi polisi ni kama wako kwenye dhamana," alisema.
Kamanda alisema kitendo cha watu kuleta bangi wenyewe kituoni kinastaajabisha kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakikamata bangi mafichoni lakini hawa wameleta wenyewe na kueleza inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina.
Tukio hilo lilitokea Februari, 25 mwaka huu, majira ya saa 11 jioni walinzi wa kampuni hiyo waliofahamika kwa majina ya Brown Jerry na Issaya Mwakalinga walikamatwa na polisi na kufikishwa kituo cha Kati Mkoa Mbeya.
Awali, ilidaiwa kuwa walikutwa na bangi nusu gunia ikiwa kavu na nyingine ikiwa mbichi.
Viongozi wa kampuni hiyo walipotafutwa kuthibitisha tukio hilo walishindwa kufanya hivyo licha ya kupigiwa simu mara kadhaa.
0 Comments