Na Mohammed Ussi
JUZI nimemsikia rafiki yangu sana Godbless Lema, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini akisema kwamba kazi ya bodaboda sio ajira, eti ni laana. Lema anayesema hayo katika mkutano wa hadhara baada ya kurejea kutoka uhamishoni nchini Canada alikokuwa anaishi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kauli hii siyo tu imewashangaza wengi wakiwemo wanasiasa wenzake, lakini imewashangaza sana vijana wengi wa nchi hii ambao wanaendesha maisha yao kupitia kazi ya kuendesha pikipiki hizi.
Wenyewe wanamshagaa Lema na wanasema kwamba wao wanaishi maisha mazuri kuliko wafanyakazi wengi wenye ajira, ama serikalini au kwenye sekta binafsi. Wanamshangaa Lema kwasababu kama wangekuwa hawana hizi bodaboda wangekuwa wanafanya nini?
Hata hivyo, kwa mwenye jicho pevu anajua kwamba vijana hawa wanaoondesha bodaboda ni jeshi kubwa sasa. Wameweza kutengeneza fursa mpya ya kulisaidia taifa katika vita dhidi ya umasikini.
Wengi wao wanafanyakazi kwa watu ambao wanawalipa kwa makubaliano maalumu, lakini wengine wameajiajiri na wanaendesha maisha yao na familia zao bila matatizo yoyote. Vijana wengi waliokuwa wanafanya matukio ya kuhatarisha maisha yao na maisha ya watu wengine leo wameachana na matukio hayo wanaendesha bodaboda.
Ama je kama isingekuwa fursa hizi ambazo serikali imezifungua za taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali, akina mama hawa wanaofanyabiashara ya mamalishe wangekuwa wanafanya biashara gani mitaani?
Ni kweli nchi imerudi kwenye joto lake la kisiasa, lakini joto hili likuwa kali zaidi ni hatari kwa maisha ya watu wengine. Juni 24, mwaka 2016 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Dkt John Magufuli aliamua kuzuia mikutano hiyo kwa nia ya kuelekeza hisia na mawazo ya kila mwanamchi kwenye kufanya kazi kwanza.
Dkt Magufuli aliamini kwamba siasa za majukwaani zilikuwa zinadumaza mawazo ya wananchi, na kwamba kwahali ya uchumi wakati ule ilikuwa jambo jema zaidi kwa wanasiasa na Watanzania wengine kuelekeza nguvu zao kwenye kufanya kazi kwanza.
Hayati Magufuli aliamini kwamba siasa zinapaswa kufanyika wakati wa kampeni tu na zikimalizika, chama kilichoshinda uchaguzi kinatakiwa kuachiwa muda wa kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa uchaguzi pasipo kukosolewa au kuzodolewa na wapinzani wake. Amri hii iliendelea kudumu hadi Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan alipotangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya kisiasa.
Mara baada ya kushika hatamu za uongozi, Rais Samia amekuwa akisisitiza kuhusu umuhimu wa kujenga taifa lenye maridhiano, ustahamivu, mabadiliko na ukuaji. Ni katika eneo la maridhiano ya kisiasa ndipo ambapo suala hili la mikutano linapoingia.
Katika muda wake wa takribani miaka miwili tu madarakani, Rais Samia ameunda Kikosi Kazi Maalumu cha kufanya mapitio ya sheria za Tanzania zinazohusu masuala ya siasa, kuvirejesha vyama siasa kwenye meza ya mazungumzo kufuatia kulegalega kwa uhusiano kutokana na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kupunguza uhasama wa kisiasa ulioanza kumea katika kipindi cha miaka iliyotangulia mwaka 2021.
Wakati huu ambapo mikutano hiyo imeanza kuna mengi yanazungumzwa. Mengine yanazungumzwa kutokana na jazba na hisia tu, lakini mengine yanazungumzwa kwasababu mitaani na kwenye viunga mbalimbali vya kisiasa kulikuwa na hoja ambazo hazikuwa zinasemwa moja kwa moja, ama kutokana na kukosekana kwa majukwaa ya kusemea, au kutokana na woga tu ambao hata hivyo ulikuwa ni woga mbaya.
Vyama vya upinzani vinaweza kuzungumza mengi kwa wakati huu. Kuna hoja ambazo zingetakiwa kufa baada ya uchaguzi mkuu wa 2020, lakini kwavile zipo na hazikuwahi kupata majibu huko nyuma, leo zinaweza kuwa kama hoja mpya. Kwa lugha nyingine wanasiasa wanatakiwa kuchagua ya kusema kwenye mikutano yao hii wasije kuonekana kuwa vituko kwenye jamii.
Hoja za kisiasa zimekuwa kama matunda ambayo yalikuwa yamevumbikwa mahali pamoja kwa muda mrefu. Kwa kipindi cha miaka saba ya siasa za Tanzania kuwa chumbani, wanasiasa wategemee kuwa baadhi ya matunda yameoza, kwa maana ya hoja zao; hivyo wanatakiwa kuchagua hoja hizo na kuangalia zipi zina mashiko kwa jamii na nyingine ni za kutupa.
Natamani kuona wanasiasa wakitumia nafasi hii kuishauri serikali ya Chama cha Mapinduzi kuyatazama baadhi ya maenei ambako bado kuna matatizo katika kuendesha gurudumu hili la maendeleo ya nchi yetu. Lakini ili waaminike na wananchi, wanasiasa hawa wawe na hoja ambazo zina mashiko, watoe yale ambayo kwa miaka saba hii yalikosa majibu.
Ni jambo jema pia kama wanachama na makada wa CCM watatumia nafasi hii kuwajibu kwa hoja wapinzani, ingawa pia kwa miaka hiyo saba CCM nao walikuwa kifungoni, japo wana nafuu kwamba wao ndiyo wameunda serikali.
Kama tumeridhia kwa pamoja kwamba sasa huu ni wakati wa kufanya siasa, basi maridhiano hayo yaonekane majukwaani kwa macho. Tuendelee kukosoana bila kuhitilafiana, lakini kama tunapingana, basi ubishi wetu usiwe chanzo cha kupigana. Bado Tanzania ni kielelezo cha siasa za kiungwana miongoni mwa nchi nyingi barani Afrika!
0 Comments