Na Noela Cosmas

MAISHA ya kawaida ya vijana wengi wa Tanzania, hasa wale ambao hawana ajira baadhi yao wamejikita kwenye tabia ambazo hazina tija katika maisha yao ya baadae ukiwemo ulevi na uvutaji wa sigara. 


Takwimu zinaonesha kwamba miongoni mwa watumiaji wengi wa dawa za kulevya, pombe na sigara, vijana wamekuwa kwenye nafasi kubwa zaidi.


Tafsiri yake ni kwamba  vijana wengi wataathirika zaidi na kwa lugha nyingine vijana hawa watakuwa wazee waathirika wa miaka ijayo.Uvutaji wa Sigara umekuwa ukitajwa kama moja ya mambo yanayohatarisha maisha kwa haraka zaidi ikiwa mvutaji atashindwa kuzingatia viwango vya uvutaji kwa afya yake mwenyewe.


Tafiti zinaonesha watu wanaovuta sigara moja kwa siku wana uwezekano wa asilimia 50 zaidi kupata magonjwa ya moyo na  asilimia 30 wa kupatwa na kiharusi kuliko watu amabo hawajawahi kuvuta sigara.


Wanaume wanaovuta sigara moja kwa siku wana uwezekano wa asilimia 48 wa kupata ugonjwa wa moyo na wana uwezekenao wa asilimia 25 wa kupata kiharusi kuliko wale ambao hawajawahi kuvuta kabisa.


Kwa upande wa wanawake, wako katika hatari zaidi asilimia 57 wanaweza kupata ugonjwa wa moyo na asilimia 31 kupata kiharusi. Hata hivyo, siku hizi kuna sigara za kieletroniki maarufu kama E-Cigarettes ambazo hizi zimekuja kuchukua nafasi ya matumizi makubwa ya tumbaku duniani na Sigara hizi zinatajwa kwamba zimeanza kutumika hapa nchini.


Lakini wataalam wa afya wanasema kwamba sigara za Kieletroniki ni hatari zaidi ya Sigara za kawaida, na katika baadhi ya nchi ikiwemo India tayari wamechukua hatua za kupiga marufuku sigara hizi.Tafiti zinaonesha kwamba Sigara za kielektroniki si salama kwa vijana, watu wazima, wajawazito, pamoja na watu wazima ambao kwa sasa hawatumii bidhaa za tumbaku.


Ingawa sigara za kielektroniki zina ladha nzuri inayotofautiana na ile ya tumbaku, lakini wanasayansi bado wana mengi ya kujifunza kuhusu ikiwa sigara za kielektroniki zinaweza kusaidia vijana kuacha kuvuta sigara.


Tayari Jumuiya ya Mabohora hapa Nchini imekuwa kwenye vikao kujadili namna ambavyo inaweza kutoa elimu kuhusiana na sigara hizi, lakini pia kuishauri serikali kuchukua hatua za haraka ikiwezekana kupiga marufuku kabisa uingizwaji wa sigara hizi.


Taarifa zinasema kwamba hata Kiongozi Mkuu wa madhehebu hayo Duniani Dkt. Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin (TUS)  ametoa maelekezo kwa Jamii kuacha matumizi ya sigara hizo hatari.


Pengine ni wajibu wa serikali yetu kupitia Wizara ya Afya kuangalia upya matumizi ya sigara hizo, na ikiwezekana kuungana na nchi ambazo zimeshapiga marufu sigara hizo kwasababu madhara yake yametajwa wazi kwamba ni hatari wa vizazi hivi na vile vijavyo. Vijana wengi wametajwa kuwa wateja wakubwa wa sigara hizi.


Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan inaweza kuendelea kufanya utafiti wa kutosha, lakini ushahidi ambao umetolewa na mataifa mengine unaotosha kuchukua hatua maana sigara hizi hazina tija kwa uchumi wa nchi.


Sigara za kielektroniki ziko katika maumbo na saizi nyingi. Nyingine zina betri, kipengele cha kufyonza, na mahali pa kushikilia kioevu.Watumiaji huvuta ‘erosoli’ iliyomo kwenye sigara hii kwenye mapafu ya na kuna ushahidi kwamba baadhi yao wamejikuta wakichanganyikiwa baada ya kuvuta sigara hii.


Sigara za elektroniki zinajulikana kwa majina mengi tofauti. Wakati mwingine huitwa "e-cigs," "e-hookah," "mods," "kalamu za vape," "vapes," "mifumo ya tank," na majina mengineyo.
Baadhi ya sigara za kielektroniki zimetengenezwa zionekane kama sigara za kawaida, sigara, au mabomba. 


Baadhi hufanana na kalamu, vijiti vya USB, na vitu vingine vya kila siku. Vifaa vikubwa kama vile mifumo ya tanki, au "mods," havifanani na bidhaa zingine za tumbaku.


Kibaya zaidi imeelezwa kwamba Sigara za kielektroniki zinaweza kutumika kuweka pia bangi na dawa zingine za kulevya, kwa mujibu wa tafiti hizo.


Imeelezwa kwamba Erosoli ya sigara ya kielektroniki ambayo watumiaji hupumua kutoka kwenye kifaa na kuitoa inaweza kuwa na vitu hatari na vinavyoweza kudhuru, ikiwa ni pamoja na Nikotini, na Kemikali zinazosababisha saratani lakini pia  ladha kama vile diacytle, kemikali inayohusishwa na ugonjwa mbaya wa mapafu.


Ni ngumu kwa watumiaji kujua ni bidhaa gani za sigara za elektroniki zinazo. Kwa mfano, baadhi ya sigara za kielektroniki zinazouzwa kuwa na asilimia sifuri ya nikotini zimegunduliwa kuwa na nikotini 2.Sigara za kielektroniki bado ni mpya, na wanasayansi bado wanajifunza kuhusu athari zao za kiafya za muda mrefu ingawa utafiti wa awali unaonesha kwamba Sigara nyingi za kielektroniki zina nikotini, ambayo ina athari za kiafya zinazojulikana. 


Nikotini iliyomo kwenye sigara hizi ni simu na inaweza kudhuru ukuaji wa ubongo wa vijana na watu wazima.Kuna ushahidi unaozidi kuonesha kuwa sigara za kieletrokoniki zinaweza kudhuru mapafu. Tarehe 17 mwezi Septemba mwaka 2019, kituo cha Marekani cha kudhibiti na kukinga magonjwa, CDCP kilianzisha uchunguzi wa dharura wa uhusiano kati ya matumizi ya sigara za kielektroniki na madhara ya mapafu na vifo.


Hadi tarehe 10 mwezi Desemba mwaka  huo wa 2019, Marekani ilikuwa imeripoti zaidi ya watu 2409 waliolazwa hospitali na vifo 52 vilivyothibitishwa kuhusiana na matumizi ya sigara hizo.
Umoja wa Mataifa unasema kwamba Takribani mataifa mengine 5 yameanza uchunguzi wa kubaini wagonjwa wa mapafu wanaohusiana na matumizi ya sigara za kielektroniki.


“Nchi zinaweza kuamua kupiga marufuku sigara hizo za kielektroniki. Tayari sigara hizi zimepigwa marufuku katika mataifa zaidi ya 30 duniani kote, ambapo nchi nyingi zaidi zinafikiria kuchukua hatua kulinda vijana” imesema taarifa ya UN kwenye mtandao wake.
 

Swali kubwa hapa ni kwamba nani ameruhusu kuingia kwa sigara hizi hatari hapa nchini, na kwa maslahi ya nani? 


Ofisa Mmoja wa Shirika la Viwango hapa nchini (TBS) ambaye anasita kutaja jina lake alipoulizwa kuhusu sigara hizi anasema ni jambo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina ambapo hata hivyo amesema ni biashara kubwa siku hizi.


Lakini uchunguzi unaonesha kwamba sigara hizo zimekuwa zikiuzwa kwa wingi maeneo ya Mlimani City, Msasani na Masaki jijini Dar es Salaam, ingawa pia zinapatikana katika makasino na maduka makubwa ya bidhaa katika maeneo kadhaa hapa nchini.


"Kusema ukweli ni vigumu kusema hadi sasa kwanini sigara hizo zipo hapa nchini, nani amezileta na madhara yake kwa ujumla" amesema Ofisa huyo wa TBS lakini akakiri kwamba hata yeye ameona hatua ambazo zimechukuliwa na baadhi ya nchi kuhusu sigara hizo.