Na Jones Mwangónda

TIMU mbili kubwa za Tanzania, Simba na Yanga zimetoka kwenye furaha ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya vilabu barani Afrika.

Simba waeendeleza rekodi yake ya kimataifa baada ya kuingia hatua hiyo kwa kishindo, safari hii wakitoa kipigo kitakatifu mbele ya Horoya FC ya Guinea kwa mabao 7-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika hatua ya makundi.

Haukuwa ushindi rahisi, lakini pia haukuwa ushindi mwepesi kwa Simba. Ni kutokana na maandalizi ya wekundu hao, lakini mipango mikakati kuanzia kwenye kikosi hadi kwa uongozi.

Simba walikuwa wanazihitaji sana alama tatu kutoka kwa Horoya, moja ya timu bora sana katika Afrika kwasasa. Lakini wangewezaje kuwafunga mabao yote saba kurahisi? Simba walipania na wamefanikiwa. 

Nawaona Simba wakifika mbali katika mashindano haya, nawaona wakifika hata nusu fainali na ikiwezekana hata fainali kabisa. Simba wajipange tu kwamba haya mabao 7 yasiishie kwa Horoya tu.

Yanga nao wameingia kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kufika rekodi hiyo.

Usajili mkubwa na uwekezaji ambao Yanga wamefanya ndiyo siri pekee ya kuwafikisha hapa. 

Huko nyuma wakati Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji anamwaga fedha na kusajili Simba, kuna watu walikuwa hawamwelewi, lakini baada ya kuona Simba wanapata mafanikio makubwa kimataifa, Yanga nao wakalazimika kuwaiga watani wao, na sasa Yanga nao wameona matunda ya uwekezaji.

Kwa kumtumia Gharib Said Mohammed "GSM" hakika Yanga wamefanikiwa. Wanaweza kuleta wachezaji wakubwa, na kama walivyofanya Simba, tayari nao wameona faida ya kusajili wachezaji wa kimataifa.

Sasa kwa mara ya kwanza, Tanzania imeingiza timu mbili kwenye hatua ya robo fainali, mafanikio ambayo huko nyuma tuliyaona kwenye nchi kama Tunisia, Morocco, Misri, Algeria na pengine wakati ule DR Kongo wakati TP Mazembe na AS Vita zikitikisa Afrika.

Uwekezaji wa Simba na Yanga umezaa matunda, anayekebehi hili anaweza kuwa na akili finyu tu.

Lakini wakati timu zetu zikipata mafanikio haya makubwa, bado tuna wasiwasi na timu yetu ya Taifa ya Tanzania "Taifa Stars" ambayo inapambana na Uganda kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Taifa Stars ina alama moja tu katika kundi lake, na inatakiwa kushinda walau michezo mitatu ili kuwa na uhakika wa kufuzu fainali hizo kwa mara ya tatu katika historia ya nchi yetu.

Unaweza ukajiuliza maswali mengi kwamba kwanini Simba na Yanga zinatisha katika Afrika lakini timu yetu ya taifa haifanyi vizuri?

Kweli, kama zilivyo nchi nyingine ambazo soka lake limekua, wachezaji wa kigeni wamekuwa na msaada mkubwa kuliko wazawa. Ndiyo maana hata ukiangalia leo msimamo wa Ligi Kuu yetu, utaona kwamba ni zile timu zenye wachezaji wa kigeni ndizo ambazo ziko nafasi za juu zaidi.

Yanga, Simba, Azam FC, Singida United zina wachezaji wengi wa kigeni, wachezaji wenye 'profile' kubwa katika soka na ndiyo maana ziko hapa zilipo.

Sitaki kuungana na wale wanaotaka tupunguze idadi ya wachezaji wa kigeni ili kunusuru timu yetu ya taifa, kwasababu zipo nchi hazina wachezaji wa kigeni kabisa na bado kiwango chake kiko chini kwenye timu za taifa.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba lazima tuongeze uwekezaji kwenye timu ya taifa, uwekezaji wa kiuchumi lakini na ushabiki wa kitaifa.

Uganda wanaotusumbua sana kwenye michezo hii ya kimataifa wamefanikiwa kutusumbua kwasababu wananchi wa Uganda wengi ni wapenzi wa timu ya taifa kuliko vilabu.

Waganda wamefanya uwekezaji kwenye timu ya taifa na wamefanikiwa kuwashawishi wananchi wao kuipenda timu ya taifa kwanza, na vilabu baadaye.

Najua kwetu sisi ni ngumu. Si rahisi kuwaambia washabiki wa Simba na Yanga waipende Taifa Stars kuliko timu zao. Wao wanajua kwamba "Yai" ni kubwa kuliko "kuku".

Lakini kama tukiamua kuanzisha hamasa upya, tukaondoa tofauti zetu na kunyoonesheana vidole kwamba huyu ni bora zaidi ya mwingine, Taifa Stars inaweza kufanya makubwa sana.

Muhimu ni kwamba tupendane na kuaminiana, lakini ushabiki wetu wa Simba na Yanga ubaki kwenye Ligi tu, linapokuja suala ambalo lina maslahi kwa nchi, tuungane.

Hata hii hatua ya Tanzania kuwa na wawakilishi wengi zaidi kwenye michuano ya kimataifa ni kama limechelewa sana. Lakini tumechelewa kutokana na ushamba wetu wa kuzishangilia zaidi timu za nje zinapokuja Tanzania na kuziacha timu za nyumbani.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba tumekuwa tukihujumiana bila sababu za msingi, matokeo yake hujuma hizo zikawa neema kwa nchi nyingine.

Lakini kama tunataka kuungana na kuwa wamoja, basi tuanzie kwenye  timu yetu ya taifa. Tuanzie mshikamano huko ili Taifa Stars ishinde, kisha turudi kwenye mshikamano huo huo kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya vilabu.

Mbona watanzania wanaoishi nje ya nchi wanashikamana pamoja bila kujali itikadi zao timu zetu zinazopokwenda huko? Hapa nyumbani tunashindwa nini?

Nimeona mara kadhaa timu zetu zinapokwenda nje ya nchi, mabalozi wetu wanazipokea na kuzipa ushirikiano, lakini pia watanzania wote wanaungana kuzishangilia bila kujali kama wao ni Simba ama Yanga.

Lakini timu za kigeni zinapokuja hapa nchini tunaanza kubaguana. Dhambi hii ya ubaguzi haiwezi kutuacha salama kama hatutabadilika.

Lakini kama nilivyosema tuanze kuungana upya, na muungano wetu uanzie kwenye timu ya taifa. Tushikamane pamoja na kuipa sapoti yetu ili ifuzu tena AFCON. Watanzania hatuna dhambi ya ubaguzi, huku kwenye michezo shetani gani anatupitia?