Na Mdoe Kiligo, MeCAP


HAKUNA asiyejua umuhimu wa makazi. Pamoja na haki nyingine muhimu kwa jamii, lakini kila mtu anayo haki ya kupata makazi, lakini sera ye serikali yetu ni kuhakikisha kwamba siyo tu kila mtazania ana haki ya kupata makazi, lakini makazi bora.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  lilianzishwa kwa madhumuni ya kumsaidia mtanzania kupata makazi. Ingawaje kuna mabadiliko ya kisheria na kisera yanayotokana na hali ya uchumi, lakini  bado madhumuni makuu ya NHC ni kuwasaidia watanzania kuwa na mahali salama pa kuishi.

Mabadiliko ya kiuchumi yamebadili mambo mengi ya Shirika hili, kasi ya ujenzi wa nyumba za kupanga na kununua imeendelea kwa kasi, na Shirika limekuwa likijiedesha kibiashara zaidi tofauti na miaka ya nyuma ambapo NHC likikuwa Shirika linalotoa huduma zaidi.

Shirika la Nyumba la Taifa la sasa ni matokeo ya uamuzi wa Serikali wa kuvunja lililokuwa Msajili wa Majumba (RoB) kupitia Sheria ya Bunge Na.2 ya mwaka 1990, iliyokabidhi majukumu yake kwa NHC. 

Iliyokuwa NHC ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya 1962, wakati RoB ilianzishwa kwa Sheria Na.13 ya 1971.

NHC ipo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara inawakilishwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo inawajibika kwa sera na mikakati ya Shirika. Kuanzia Julai, 1994,  Shirika lilijielekeza kwenye jukumu la kujenga na kuuza nyumba zaidi ili kwenda na kasi ya ukuaji wa uchumi, lakini pia maendeleo ya makazi kwa ujumla.

Ongezeko la watu hapa nchini na hasa kwenye miji limefanya mahitaji ya nyumba kuwa makubwa zaidi. Miji imekuwa mikubwa zaidi, na watu wanaohitaji nyumba wamekuwa wengi pia.

Nyumba za watu binafsi zimekuwa na changamoto kubwa ambapo wenyenyumba hizo wamekuwa wakipangisha nyumba zao kwa bei ambazo hazilingani na kipato cha mtanzania wa kawaida leo.

Lakini kama haitoshi, kabla ya kupata nyumba madalali wamekuwa wakinufaika zaidi kwa kupata fedha za bure kutoka kwa wapangaji wanaohitaji nyumba, jambo ambalo liliwahi kupigwa marufuku na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, lakini hadi sasa kero hiyo imeendelea kuwaumiza wapangaji.

Kero hii ya madalali imeumiza na inaendelea kuumiza watu wengi, hasa pale wanapotaka walipwe kodi ya mwezi mmoja na wapangaji kama ujira wa kuwatafutia makazi. Huu ni wizi, ni uonevu ni ujambazi wa mchana ambao serikali inatakiwa ipambane nao.

Kweli madalali wanatakiwa wapewe ujira kutokana na kuwasaidia wapangaji kupata nyumba, lakini anayetakiwa kuwalipa madalali hao hatakiwi kuwa Mpangaji, ndiyo maana wakati ule Lukuvi alikuwa mkali kwenye hili.

Hata katika mifumo ya mapato ya kawaida, anayeuza ndiye anatakiwa kulipa asilimia fulani kwa mtu ambaye amesimamia mauzo hayo, awe dalali au mtu mwingine. Kwanini kwenye hili la nyumba mpangaji ndiye anaumia? Serikali ina jambo la kufanya, isiwe kama Mhe. Lukuvi amemaliza utumishi wake na agizo lake nalo limemalizika pia.

Kwangu mimi naamini kwamba NHC wanaweza kuondoa uhuni huu wa madalali ikiwa watajenga nyumba nyingi za kupangisha huku wakiwa pia kwenye lengo lao la kujenga nyumba za kuuza.

 Juzi nimemsikia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda akitaka kuwapo mabadiliko makubwa katika nyanja zote za utoaji huduma kwa Watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa ili waweze kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Nimevutiwa na hotuba ya Naibu Waziri huyo kwakuwa inaonesha kwamba serikali ya Rais wa awamu ya sita, Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza kero ya makazi hapa nchini, na kuona kwamba kila Mtanzania anapata makazi bora kwa ustawi wa maisha yake.

Naibu Waziri Pinda ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya siku moja kufahamu kazi zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuzungumza na Wafanyakazi wa Makao Makuu kwa niaba ya Wafanyakazi wote wa Shirika.

Naibu Waziri Pinda akasema: “Nichukue nafasi hii kuwapongezeni kwa kazi kubwa mnazozifanya kwa maendeleo ya Taifa, lakini niwachagize kuwa tunataka mabadiliko makubwa ya utoaji huduma ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa kila mmoja kufanya kazi apaswayo, mpendane, mheshimiane na mthaminiane na sisi kama Serikali tutawaunga mkono kama mlezi wenu,".

Ameutaka uongozi wa Shirika hilo kuutumia ujuzi wa Mkurugenzi Mkuu ambaye ameteuliwa akitokea katika uongozi kwenye taasisi ya sekta binafsi ili Shirika liweze kukua kwa kasi kibiashara kama linavyotakiwa.

“Fanyeni sensa ya kutambua nyumba zenu nchi nzima na mpitie mikataba yenu na wapangaji kuwe na utafiti wa mahitaji ya nyumba maeneo mbalimbali nchini kuna wapangaji wenu wanawapangisha watu wengine kwa fedha nyingi huku wakilipa NHC fedha kidogo, hili siyo jambo jema,”amesema.

Ametaka kuongezwa kasi ya kudai kodi kwa wadaiwa sugu wa Shirika hilo na kwa zile taasisi za Serikali ambazo nazo ni wadaiwa sugu orodha yao iwasilishwe Wizara ya Ardhi ili kusudi Wizara isaidia kudai kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amependekeza pia uanzishwaji wa vijiji vya mfano vyenye kuleta tija lakini vyenye kuwasaidia Watanzania waliopo pembezoni pamoja na kwamba Shirika linaendeshwa kibiashara .

Ameelekeza ushirikishwaji wa Wafanyakazi wote kwa Menejimenti inapoamua kuyabuni mawazo ya maendeleo. 

“Mimi nataka ustawi wa watumishi pia muwape malengo, watekeleze majukumu yao wanayotakiwa kuyatekeleza, lakini pia wapewe motisha ya kutosha ili kuwa na tija kwa nchi".

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah alielezea umuhimu wa Serikali kulisaidia Shirika ili kuhakikisha kwamba Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora.

“Kadri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka, uhitaji wa makazi unaongezeka pia. Idadi ya Watanzania inaongezeka kwa asilimia 3.1 kila mwaka ambayo inapelekea kuzidi kwa upungufu wa nyumba za makazi nchini. Hadi sasa kuna uhitaji wa nyumba milioni tatu na laki nane za nyumba za makazi nchini,” amesema Hamad.

Hamad amesema kuwa miaka ijayo asilimia 48 ya Watanzania wote watakuwa wanaishi mijini hivyo kuna haja kubwa ya kuongeza idadi ya makazi katika miji na nchini kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali haina budi kuunga mkono juhudi za Shirika katika uendelezaji wa miliki kwani kwa kupitia utekelezaji wa shughuli tofauti za Shirika kuna manufaa tofauti kama vile upatikanaji wa ajira kwa Watanzania, kuongezeka kwa pato la Shirika kupitia uuzaji na upangishaji wa nyumba na taasisi nyinginezo kama vila Tanesco na DAWASA na pia inachangia kwa kiasi kikubwa katika uendelezaji wa viwanda nchini kwani ujenzi wa nyumba unajumuisha matumizi ya bidhaa za ujenzi kama vile nondo, mabati, saruji n.k

“Riba kubwa zinazotozwa na mabenki pindi wananchi wanapochukua mikopo ya ujenzi asilimia 14 hadi 20 pamoja uwezo mdogo wa kiuchumi wa Watanzania wengi ni mojawapo kati ya changamoto zinazozuiya ukuaji wa sekta ya nyumba,” alisema Hamad.

Alieleza kwamba idadi kubwa ya Watanzania wana vipato vidogo hivyo, riba ya asilimia 14 hadi 20 ni kubwa kwao pindi wanapochukua mikopo benki.

Pia hakusita kueleza jinsi Shirika lilivyomudu kuwapatia wanunuzi wake mikopo ya nyumba kwa riba ya asilimia 9 kwa Watanzania wanaonunua nyumba Iyumbu, Dodoma.

Nina uhakika NHC wakijenga vijiji vya mfano kama alivyoshauri Naibu Waziri, tatizo la makazi katika nchi hii litakuwa historia.