Na Anania Njonjo

Kampuni ya Usafirishaji ya Safari Haulier ya jijini Dar es Salaam, inadaiwa kumiliki pampu na kisima cha mafuta kwenye yadi ya kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na blogu hii hivi karibuni, umebaini kuwepo kwa pampu ya mafuta katika yadi ya kampuni hiyo iliyoko maeneo ya Kipawa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Uwura), imetoa muongozo kwa umma kuwa ni marufuku kwa mfanyabiashara au mtu yoyote kufunga pampu na kuweka kisima cha mafuta kwenye maeneo ambayo yasiokuwa vituo vya mafuta.

Agizo hilo limetolewa chini ya sheria ya Mafuta Cap.392 ya Mwaka 2018 inayoelekeza kununi na taratibu za biashara ya uuzaji wa mafuta ya jumla, uhifadhi, ukarabati na ufungaji wa pampu za mafuta na adhabu ya atakayekiuka sheria hiyo kuwa ni faini isiyopungua milioni 20.

Licha ya kampuni hiyo uchunguzi wa blogu hii umebaini kuwa kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara wa mafuta wamefunga pampu za mafuta katika yadi, gereji na kinyume cha sheria hiyo.

Aidha, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuuza mafuta katika yadi bila kulipa kodi za mapato kwa kutotoa lisiti za EFDS hivyo kukwepa kulipa kodi.
 

Mwandishi wa habari hii, alifika kwenye yadi ya kampuni hiyo na kushuhudia pampu hiyo ya mafuta na kuongea na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina mmoja la Ahmed akiwa kama Operesheni Ofisa.

Akizungumza na Morningstar Post, Bw Ahmed alisema vibali vyote vya ufungaji wa pampu na kisima vya mafuta viko ofsini kwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ambaye wakati huo alikuwa yuko nje ya nchi.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alipopigiwa simu alijibu kwa mkato akiwataka mwandishi wa habari hizi kwenda kupata maelezo zaidi kuhusu pampu hizo Ewura.

"Nendeni Ewura wanajua kila kitu", alisema mkurugenzi huyo ambaye alikataa kujitambulisha na kukata simu.

Meneja Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo, alisisitiza kuwa Ewura haitoi vibali wala ruhusu ya kufunga pampu ya mafuta kwenye viwanja na maeneo yasioyokidhi vigezo.