Na Jones Mwangonda

Mtu mmoja raia wa Comoro, aliyefahamika kwa jina la  Ali Mohamed (66), amejirusha kutoka juu ya ghorofa ya tisa na kufariki dunia.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana usiku mtaa wa Amani jijini Dar es Salaam kwenye jengo la Amani resindensy lililoko mtaa wa Amani ambako marehemu alikuwa amepanga.
 

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Jumanne Mulilo.

Akizungumza na Morningstar POST Kamanda Mulilo alisema ni kweli wamepokea taarifa za tukio hilo na kubaini kuwa marehemu alijirusha toka ghorofani kutokana na matatizo ya akili.

"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa na matatizo ya akili, alisema Kamanda Mulilo.

Akizungumza na Morningstar POST, mfanyakazi wa marehemu huyo alijitambulisha kwa jina la Said Swalehe, alisema kuwa marehemu alikuwa na tatizo la kupandwa na mashetani mara kwa mara.
 

Bw. Said akaongeza kuwa mwaka jana alitenguka mgongo alipofanya jaribio la kujirusha kutoka ghorofani katika jengo la Sembenua Lakisale lililoko Comoro na kumsababishia matatizo ya mgongo yaliopelekea kuletwa hospatali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
 

"Akipandisha mashetani ndio huwa anafanya majaribio ya kujirusha, hali hii imekuwa ikimtokea mara kwa mara," alisema Bw Said ambaye nae ni raia wa Comoro aliyekuja jijini Dar es Salaam na marehemu kwa ajili ya kumuhudumia.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hosptali ya Taifa Muhimbili ukisubiri kusafirishwa kuelekea Comoro mara baada ya ndugu wa marehemu kuwasili jijini Dar es Salaam, wengine wakitokea Ufaransa.