Na Mwandishi Wetu
KASI ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo imeanza kuwatisha baadhi ya watendaji wa serikali ya chama hicho, baadhi yao wakihofia kupoteza nafasi zao.
Katibu Mkuu huyo wa CCM amekuwa kwenye ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na serikali, na katika baadhi ya maeneo amehoji kuhusu uzembe ambao hauendani na dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu Mkuu huyo wa CCM amekuwa mkali kwenye kusuasua kukamilika kwa miradi mbalimbali, lakini uzembe kwenye utoaji huduma za kijamii na kuwataka wasimamizi wa maeneo hayo kufanya kazi zao kwa umakini ili wananchi waone matokeo chanya.
Amewataka viongozi wa serikali kuanzia Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kufanya kazi zao kwa maslahi mapana ya nchi na kuacha kufanya kazi mazoea.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya CCM kimesema kwamba kasi ya Katibu Mkuu huyo imekuwa ikiwatisha baadhi ya viongozi kutokana na wasiwasi kwamba wanaweza kutumbuliwa wakati wowote.
"Siku hizi mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na hata wakurugenzi wengi wamekuwa na wasiwasi kwamba wakienda nje ya mstari wanaweza kutemwa kwenye nafasi zao, na hasa wakimtazama Rais Samia ambaye hakupi uhakika wa kubaki kwenye eneo lako la kazi kwa wakati wote" kimesema chanzo hicho.
Rais Samia amekuwa akipangua mawaziri na viongozi wengine wa serikali na hivi karibuni alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri lakini pia akiwahamisha baadhi ya viongozi wengine.
Dkt Samia amesema kuna wakati kumekuwa na kutoelewana miongoni mwa watendaji wa serikali, na sababu hiyo ni mojawapo ya chanzo cha kuhamishwa ama kutumbuliwa kwa baadhi ya watendaji hao.
Rais amesema kwamba hii itakuwa mara ya mwisho kutumia sababu hiyo kuwabadilisha vituo vya kazi baadhi ya mawaziri na watendaji wengine wa kazi, na kwamba ikitokea hivyo mara nyingine atawaondoa wote.
Wadadisi wa mambo wanasema kwamba Chongolo amejipambanua na watangulizi wake katika nafasi hiyo nyeti, ambao staili yake ya kuwabana mawaziri na viongozi wengine wa serikali ya CCM inakisaidia Chama chake kuaminika kwa wananchi.
"Huyu ni Katibu Mkuu wa Chama tawala, chama ambacho kimeshika dola ya nchi. Yeye ndiye mtendaji mkuu wa taasisi ambayo imeshikilia moyo wa nchi, lazima awe mkali ikiwa anaona kuna mambo hayaendi sawa.
Mawaziri na watendaji wengine wamezoea kuona hoja zinazohusu utendaji wao zinaguswa kwenye vikao vya kiserikali, wengi hawajui kwanini walipewa ilani ya chama chao wakati wanaapa kuitumikia nchi" amesema Dkt Sebastian Mashaka, mmoja wa wanazuoni wabobevu wa masuala ya siasa na uchumi.
"Raha ya siasa ni kwamba hata kama Waziri ana misuli kiasi gani lakini lazima awe mpole kwa Katibu Mkuu wa chama chake maana yeye ndiye anashikilia hatima ya Waziri huyo. Leo Chongolo akitoa mapendekezo yake kwa mamlaka za uteuzi kwamba Waziri fulani, ama Naibu wake au Mkuu wa mkoa na kadhalika ameharibu katika utendaji wake, ikithibitika hivyo, kiongozi huyo anaondoka.
Kwa hiyo mawaziri wetu lazima wajue kuwa wana Katibu Mkuu wa chama ambaye hakai ofisini, muda wote yuko eneo la tukio" amesema Dkt Mashaka.
0 Comments